Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zubeir kuzitumbua taasisi za Hijja
Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally amezitaka taasisi zilishiriki katika usafirishaji mahujaji kwenda Hija mjini Makka nchini Saudi Arabia kurudisha fedha kwa watu wote waliyokwama kupata safari hiyo ndani ya miezi sita kutokea sasa.
Akizungumza katika baraza la Eid al- adha iliyofanyikia katika msikiti wa Taqwa Ilala Bungoni Jijini Dar es Salaam leo amewahakikishia mahujaji waliyokosa safari kuwa pesa zao hazitoweza kupotea bure.
"Tunawahakikishia mahujaji waliokwama kwamba haki zao hazita potea, pesa zao ni lazima zirudishwe ili waweze kupata fursa ya kupata Hijja mwakani (2018). Huenda mwaka huu haukuwa wao, lakini pia isiwe sababu ya kupotea pesa zao kwa hiyo makubaliano yetu ni kama nilivyosema kwamba taasisi husika zitalipa pesa zote za mahujaji ndani ya miezi sita kutoka sasa ili kutoa fursa ya maandalizi ya mahujaji kwa wakati muafaka", alisema Mufti.
Pamoja na hayo, Mufti Mkuu amesema ipo haja ya kuzipitia upya taasisi zote zinazojishughulisha na masuala ya usafirishaji watu ili waone kama zinasifa ya kuweza kufanya hivyo na endapo watazibaini hazina vigezo basi zitachukuliwa hatua stahiki.
"Nimelazimika kuunda tume maaalum itakayoleta mapendekezo kwangu ya kuziba mianya yote inayopelekea kutokea aibu hii kujirudia kila mwaka katika msimu wa hijja unapoingia.
Hata hivyo nimeona ipo haja ya kuangalia upya taasisi ambazo hazikidhi vigezo ambazo zinaleta usumbufu mara kwa mara zitachunjwa na kuzuiwa kufanya kazi ya kupeleka mahujaji pamoja na kufutiwa usajili wake", alisisitiza Mufti.
Kwa upande mwingine, Mufti Mkuu amewapa pole mahujaji pamoja na familia zao zilizoshindwa kutekeleza ibada hiyo kwa mwaka huu.
Post a Comment