Header Ads

Mradi wa Taka ulioasisiwa na Meya wa Chadema wakubaliwa



Serikali imeridhia ombi la msamaha wa kodi iliyoombwa na Manispaa ya Kinondoni kuhusu vifaa vya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata taka na kuwa mbolea kitakachojengwa eneo la Mabwepande.

Kiwanda hicho, kitakachojengwa kwa miezi 12 na kugharimu zaidi ya Sh4 bilioni, kinafadhiliwa na Jiji la Humburg la Ujerumani na kitazalisha mbolea itakayotokana na malighafi ya taka za masoko ya manispaa hiyo.

Mradi huo ulitangazwa Januari mwaka jana na aliyekuwa meya wa manispa hiyo, Boniface Jacob lakini ulikwama kwa madai kwamba manispaa hiyo haikuishirikisha Wizara ya Fedha na Mipango na badala yake iliwasiliana moja kwa moja jiji la Humburg.

Hata hivyo, Jacob ambaye hivi sasa ni Meya wa Ubungo alinukuliwa na gazeti hili akisema kuwa hatua ya Serikali kutaka vifaa hivyo kulipiwa kodi zilikuwa njama za kuukwamisha mradi huo usitekelezwe chini ya uongozi wake na kwamba zaidi ya Sh800milioni zilikuwa zikihitajika kama kodi.

Lakini jana, Meya wa Kinondoni (CCM), Benjamin Sitta aliwaambia wanahabari kwamba chini ya utawala wake walianzisha upya mchakato huo kwa kuishirikisha wizara hiyo ili uwemo katika kumbumbuku zake na hatimaye ikaridhia ombi lao.

“Mwanzoni waligoma siyo kwa nia mbaya, sasa hivi sera zimebadilika, ili kupata msamaha wa kodi, miradi yote lazima isajiliwe Wizara ya Fedha. Ndiyo Humburg waligoma kutoa kodi kwa sababu siyo uungwana watoe msaada wa vifaa vya kiwanda viliyotokana na fedha za wananchi wao halafu watumie asilimia kubwa kulipa kodi.

“Ndiyo maana tuliamua kuanzisha upya mchakato huu na kurebisha pale tulipokosea. Namshukuru Rais John Magufuli kwa sababu Wizara ya Fedha imekubali na ikatupa utaratibu wa kuingiza mradi huu kisha kuusajili, tukatengeneza mpango ambao ulihusisha Serikali Kuu kisha Waziri wa Fedha na Mipango akasaini,” alisema Sitta.

Alifafanua kwamba mradi ukisainiwa na manispaa kwa manispaa au jiji kwa jii bila kuishirikisha Serikali Kuu hauwezi kupata msamaha wa kodi.

Sitta ambaye pia ni Diwani wa Msasani, alisema mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi huu na kwamba makubaliano ni kuwa Humburg itaugharimia na kuuendesha kwa mwaka mmoja ikiwajengea uwezo wataalamu wa manispaa wa kuuendesha.

“Katika makubaliano ya mradi huu, manispaa imetoa kiwanja cha ekari 14, kugharamia miundombinu ya barabara, maji na umeme. Kiwanda hiki kikikamilika kitapunguza tani 180 za taka zinazozalishwa kila siku katika masoko ya manispaa hii,” alisema.

Mshauri mtaalamu wa mradi huo, Dk Florian Koelch alisema wanafurahia hatua hiyo na wapo tayari kwa ajili ya kuanza kazi kujenga kiwanda hicho baada ya taratibu zake kukamilika.

No comments