Header Ads

Wananchi wasimamisha msafara wa Magufuli

                                               Rais John Pombe Magufuli

Msafara wa rais John Pombe Magufuli ulisimamishwa na raia ulipokuwa ukielekea Jijini Dar es Salaam kutoka Dodoma, wakielezea kero zao kuhusu maafisa wa manispaa ya Morogoro .

Wanachi hao waliojawa na ghadhabu walimlalamikia rais kuhusu vile wanavyohangaishwa na askari wa manispaa ya eneo hilo hususan katika maeneo wanayofanyia biashara baada ya kituo cha mabasi cha msamvu kujenga upya.

Akiwahutubia rais Magufuli aliwaagiza viongozi wa manispaa ya eneo hilo pamoja na viongoizi wa mkoa wa Morogoro kuwaacha wafanyabiashara ndogondogo wa mji huo waendelee kufanya biashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.

Vilevile rais Magufuli alimuagiza kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Onesphory Matei kuhakikisha askari mgambo hawasumbui wafanyibiashara hao huku akiwashauri wafanyibiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amewataka watu wote waliobinafsishiwa viwanda mbalimbali katika mkoa wa Morogoro kuvirejesha Serikalini endapo wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajira.

"Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu" amesisitiza Magufuli.

Rais Magufuli amewapongeza wakulima wa mazao Mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na amewataja wakulima wa Wilaya ya Kilosa kwa kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 msimu uliopita hadi kufikia asilimia 82 katika msimu huu.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi, lakini amewataka waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.

No comments