Header Ads

Yanga kuwakosa Chirwa na Mwashiuya



YANGA itawakosa wachezaji wake nyota, viungo washambuliaji Mzambia Obrey Chirwa na mzawa Geoffrey Mwashiuya katika mchezo wa kirafiki kesho dhidi ya Singida United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana kusumbuliwa na maumivu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam, Msemaji wa Yanga, Dismas Ten amesema kwamba pamoja na kwamba wawili hao watakosekana, lakini wachezaji wengine wote wapo vizuri kuelekea mchezo huo wa kwanza wa timu hiyo kujipima nguvu baada ya maandalizi ya msimu mpya kwa takriban mwezi mmoja.

“Singida United ni timu nzuri na imefanya usajili mzuri, hivyo mechi ya kesho itakuwa na ushindani mkubwa na tunawaomba wapenzi na mashabiki wajitokeze kwa wingi kesho uwanjani kuisapoti timu yao na tunawaahidi timu yetu itafanya vizuri, amesema Ten.

Msemaji huyo wa Yanga ametaja viingilio katika mchezo huo vitakuwa ni Sh.15,000 kwa VIP A, 10,000 kwa VIP B na C na majukwaa mengine yote yaliyosalia itakuwa ni Sh. 3,000.

Awali ya hapo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba wameachana na kiungo Mzambia, Justine Zullu baada ya kushindwa kufanya vizuri katika kipindi cha nusu msimu wa kuwa na klabu hiyo kwenye mkataba wake wa mwaka mmoja.

Mkwasa amesema wapo kwenye mazungumzo na mchezaji huyo ili waachane vizuri, kuliko kesi hiyo kufikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

“Zullu sisi bado tuna mkataba naye wa mwaka mmoja ila tutakaa na meneja wake meza moja tuweze kukubaliana naye ni kiasi gani cha gharama cha kumrudishia ili tuachane salama kuliko mambo ya kupelekana FIFA,”amesema Mkwasa.

No comments