Viongozi wa vijiji wakwaa tuhuma nzito
WANANCHI wa Kijiji cha Visezi Kata ya Vigwaza wilayani Bagamoyo, wameutuhumu uongozi wa kijiji hicho kwa kufanya ubadhilifu wa Sh. milioni 32 zilizotokana na kuuzwa kwa ekari 40 za mashamba ya kijiji.
Mbali ya ubadhilifu wa fedha hizo, pia uongozi huo umetuhumiwa mara kadhaa kuuza holela wa mashamba ya kijiji bila ridhaa ya wanakijiji.
Wakizungumza na Nipashe juzi, baadhi ya wananchi walisema awali walikubaliana kuuza ekari hizo ili kupata fedha kwa ajili ya kujenga nyumba mbili za walimu lakini baada ya kuuza, hakuna kilichoendelea wala taarifa waliyopewa.
"Ikabidi kwa kushirikiana na diwani wetu tukamsimamisha mwenyekiti wa kijiji, Hamis Kitala,
kutokana na tuhuma hizo, ili kupisha uchunguzi," alisema Adamu Mohamed.
Walisema malalamiko hayo yalimfikia Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, ambaye aliamua kusimamisha uongozi wote wa kijiji na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi na akawaahidi ndani ya wiki mbili kurudisha majibu.
"Tulisubiri ripoti ya Takukuru hadi Leo hatujapata, badala yake Ofisa Tarafa alikuja akaitisha mkutano na kusema ametumwa na DC (Mkuu wa Wilaya) arudishe uongozi madarakani.
Tulipouliza ripoti ya Takukuru alisema kazi iliyomleta ni kurudisha uongozi madarakani na hataki maswali," alisema Ramadhani Rajabu.
Walisema kwa sasa hawaelewi kinachoendelea kwa kuwa hawajui ripoti ya Takukuru ilibaini nini na kuwa hawaridhishwi na kurudishwa kwa uongozi bila maelezo yoyote, wakati wana tuhumiwa kwa ubadhilifu.
“Tangu mwaka jana DC alisema angerudi tena Desemba Mosi, mwaka jana kwa ajili ya kutuletea ripoti ya Takukuru. Matokeo yake uongozi umerudishwa bila maelezo halafu tunaona msingi tu umejengwa.
Kwa kweli tunaomba Rais (John Magufuli) wetu mtetezi wa wanyonge atusaidie sisi wananchi wa Visezi,” alisema Adamu Mtonga.
Mwenyekti wa Kijiji, Kitala, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alisema ni kweli alisimamishwa ndani ya miezi mitatu kwa tuhuma ambazo si za kweli na kuwa baada ya uchunguzi ilibainika hana hatia ndiyo maana mkuu wa wilaya alimrudisha madarakani.
“Wakati napata nafasi ya uenyekiti nilikuta ardhi ya kijiji inauzwa ovyo na mimi nikaja na msimamo wangu wa kuzuia ndiyo maana nimekuwa adui wa watu wanaotegemea kuendesha maisha yao kwa kuuza ardhi.
Hizi tuhuma za kuuza ekari 40 si kweli, hakuna kitu kama hicho.
Hizi ni chuki binafsi, kama unataka niitishe mkutano wa wanakijiji uwahoji ukweli juu ya jambo hili”, alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Post a Comment