Bomoabomoa nyingine kutikisa Dar
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), limesema wakati wowote litaendesha operesheni ya kubomoa nyumba zote zilizojengwa kando ya Bonde la Mto Msimbazi kinyume cha sheria.
Operesheni hiyo itawahusu pia wale wote waliojenga vibanda katika Bonde la Mkwajuni eneo la Magomeni wilayani Kinondoni.
Akizungumza na wanahabari leo Agosti 28 katika eneo la Mto Msimbazi, Mwanasheria Mwandamizi wa Nemc, Manchare Heche amesema watu wanaoishi katika maeneo hayo wanatakiwa kujiandaa kuondoka katika bonde hilo.
Amesema wanaoishi eneo hilo wanavunja utaratibu kwa kuwa ni sehemu hatarishi kwa maisha yao na kwamba, walishapigwa marufuku lakini baadhi wamerudi kinyemela.
"Mfano hawa wenye vibanda ambavyo vinachomoza kila kukicha katika Bonde la Mkwajuni, tulishawapiga marufuku na hapa palikuwa peupe lakini wamerudi.Sasa nawaambia wajiandae kuondoka hapa, operesheni hii itawahusu,"amesema.
Alipoulizwa bomoabomoa inaanza lini, Heche hakutaka kusema zaidi ya kusisitiza wananchi wajiandae kuondoka ili kupisha operesheni hiyo.
Post a Comment