Header Ads

Kabla Ya Kufanyia Kazi Ushauri Wa Kibiashara Unaopewa, Zingatia Haya

Kama kuna kitu ambacho kila mtu anaweza kushauri kadiri ya utashi wake, basi ni ushauri wa kibiashara. Watu wengi wamekuwa wakipokea ushauri wa biashara unaotolewa na kila mtu, tena kwa bure, lakini wanapoufanyia kazi ndipo wanagundua haukuwa ushauri mzuri.

Kila kipindi kuna aina za biashara ambazo huwa zinashabikiwa na watu wengi, biashara ambazo kila mtu anaongelea na wale wanaozifanya kuonekana waipata faida. Hapa ndipo unakuta kila mtu anashauriwa kuingia kwenye biashara hiyo, kwa sababu ndiyo ‘habari ya mjini’ kwa wakati huo na hivyo wengi wanakimbilia kuchukua hatua kabla fursa haijawapita.

Changamoto nyingine kubwa inayowafanya watu kupewa ushauri ambao siyo makini kwenye biashara ni kutokuwa tayari kulipa gharama za ushauri. Wengi wamekuwa wakichukulia ushauri kama kitu kidogo ambacho hakipaswi kulipiwa. Hivyo wanachukua ushauri wa bure ambao unawaumiza sana.

Leo tutakwenda kujifunza mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kufanyia kazi ushauri wowote unaopewa kibiashara. Kwa kuzingatia mambo haya utaepuka kufanya maamuzi ya msukumo ambayo yatakuingiza kwenye hasara.

Jambo la kwanza; fanya utafiti wako mwenyewe.
Usipokee maneno ya watu na kuyaamini kwa asilimia mia moja. Fanya utafiti wako kujua kama kweli biashara unayoambiwa inalipa kama ni kweli. Angalia ukubwa wa soko la biashara hiyo, ona ni kwa kiasi gani bado wateja hawajafikiwa. Pia angalia uwezekano wa kukua zaidi kwenye biashara hiyo. Fanya utafiti wako mdogo kulijua soko na hata kuwajua wale waliopo kwenye biashara hiyo kwa sasa.

Jambo la pili; ongea na wale wanaofanya.
Kwa kuwa umesikia biashara inalipa, usifikiri kwamba haina changamoto zake. Na ili kujua changamoto za biashara yoyote, angalia wale ambao wanafanya biashara hiyo. Ongea nao au wafuatilie ili kuona changamoto yao hasa ni nini. Ni vyema ukazijua changamoto za biashara yako mapema kabla hata hujaingia ili uweze kupambana nazo.

Wengi wa wanaoshindwa kwenye biashara mpya ni kutokana na kukutana na changamoto ambazo hawakuzitegemea hapo awali.

Jambo la tatu; mwangalie yule anayekupa ushauri wa biashara.
Watu wengi wamekuwa wakitaka kusikia tu ushauri mzuri wa biashara, hivyo wakiusikia hawajali anayewaambia ni nani. Hivyo unakuta mtu kasikia wengine wanasema biashara fulani inalipa, na yeye anatoka na taarifa hizo kuja kukupa wewe. Hajafanya utafiti wowote na wala hana utaalamu wa biashara, ila amesikia inalipa na anakuambia na wewe ukafanye kwa sababu inalipa.

Hakikisha mtu unayechukua ushauri wa biashara kwake ana utaalamu wa biashara au anafanya biashara hiyo anayokushauri ufanye. Kama na yeye amesikia inalipa ila hajui kwa kina kuhusu biashara hiyo, ni vyema ukaokoa muda wako au kufanya utafiti zaidi kabla hujaingia kwenye biashara hiyo.

Ni rahisi kushauri kuliko kufanya, hivyo mara zote unapopokea ushauri chunguza kwa makini kabla hujachukua hatua. Usiharakishe kufanyia kazi ushauri unaopewa kwa sababu tu unaonekana ni biashara itakayokulipa. Fanyia kazi ushauri unaopewa na utoke na mpango ambao unaweza kuupigania mpaka kufanikiwa kwenye biashara yako.

No comments