Hausigeli amchoma moto mtoto wa bosi
House Girl anayedaiwa kufanya tukio hilo.
Inasikitisha! Hausigeli aliyetajwa kwa jina moja la Maua anashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Yusufu kwa kudaiwa kumchoma moto mdomoni, mkononi na kumpiga kwa mwiko kwenye uti wa mgongo, mtoto wa miaka miwili aitwaye Nasra.
NI KIMARA DAR
Tukio hilo la kusikitisha, limetokea hivi karibuni maeneo ya Kimara- Bonyokwa jijini Dar, nyumbani kwa bosi wa hausigeli huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mama Karan.
SIMULIZI YA UCHUNGU
Akisimulia kwa uchungu, mama wa mtoto huyo, mama Karan, alianza kwa kuelezea jinsi alivyompata hausigeli huyo na kusema kwamba amesikitishwa na kitendo cha kinyama alichokifanya binti huyo.
MSIKIE MAMA KARAN
“Msichana huyu nililetewa na rafiki yangu kutoka Morogoro, alikuwa hajamaliza hata mwezi mmoja tangu afike. “Alipofika kwa mara ya kwanza alionesha kuwapenda sana watoto mpaka nikamuamini na kuondoa wasiwasi, nikawa naenda kazini na kuwaacha watoto nikirudi nawakuta salama na kila kitu kipo sawa.
UPEPO WAGEUKA…
“Baada ya kupita kama wiki hivi, watoto wangu walianza kunililia, wa kiume mwenye miaka 5 na wa kike mdogo mwenye miaka 2. “Mkubwa ndiyo akawa analia sana na kuniambia mama usiende kazini nikamuita dada mbele yao na kumuuliza kwani dada unawapiga watoto? Mbona wananililia? Nikamuuliza na mtoto mkubwa akawa haongei, anamuangalia dada muda mwingi,” alisema mama Karan.
Akizidi kuzungumzia tukio hilo huku mara kadhaa akitokwa na machozi, mama Karan alisema baada ya kuona kitendo hicho, alipata shaka. “Nilihisi kuna tatizo, nikawaita majirani zangu mbele yake na kuwaambia watoto wanavyonililia na jinsi nilivyohisi kuna jambo limetokea. “Wakaniahidi kuwaangalia watoto kama kuna jambo baya wangenifahamisha.
Niliendelea na kazi bila wasiwasi kwani nilijua kama kuna kitu kinachoendelea nitafahamishwa,” alisema mama huyo.
HAUSIGELI AIFUNGA SIMU YA BOSI
Mama Karan alisema, siku chache baadaye, baada ya kuona majirani watakuwa wakimtonya matukio yake kwa simu, aliomba simu ya bosi wake kijanja na ‘kuibloku’. “Baada ya siku chache nimerudi nyumbani dada akaniomba simu yangu ya mkononi na kuniambia kuwa simu yake haina vocha anaomba aongee na dada yake, nilimpa sasa sijui aliifanya nini maana baada ya hapo sikupata tena simu yoyote. Aliiblok kila sehemu nilipomuuliza akaniambia kuwa yeye hajui kuitumia inawezekana amegusa sehemu ambayo siyo. “Sikujali nilikwenda kazini lakini pia nilimwambia mume wangu ili aje aitengeneze lakini kabla haijatengenezwa ndiyo tatizo likatokea,” alisema.
SIKU YA TUKIO
Mzazi huyo alizidi kuelezea tukio hilo kwamba siku binti huyo alipofanya unyama huo, alichelewa kupata taarifa kwani simu yake ilikuwa haipo hewani. “Siku ya tukio nilikuwa kazini kumbe nyumbani watoto wanapigwa sana na dada yao majirani walikuwa wakinitafuta lakini hawakunipata.
“Nakumbuka ilikuwa siku ya Jumamosi (iliyopita) nilipotoa tu mguu kwa maelezo ya majirani aliyeanza kupigwa alikuwa ni mtoto wangu mkubwa akaomba msamaha akahamia kwa mdogo akampiga sana, kaka yake akaanza kumuomba amsamehe lakini akachukua rungu na kumpiga kisha akamwambia anyamaze.
KIPIGO KIKAENDELEA
“Kipigo kwa mtoto mdogo kiliendelea wakawa wanalia kwa sauti huku mkubwa akimuombea msamaha mdogo wake kwani alikuwa akimpiga na mwiko mpaka akauvunja.
AWANYAMAZISHA KWA KUWATISHIA MOTO
“Wakati wakiendelea kulia msichana huyo aliwaambia atawachoma moto wakiendelea kupaza sauti.
MAJIRANI WAINGILIA KATI
“Majirani waliposikia kelele walikwenda kumuita msichana huyo wakimsihi kufungua mlango kwani alikuwa amewafungia kwa ndani ili mtu asifungue lakini aliwaambia hayawahusu. “Huwezi amini, jirani mmoja alifika akagonga mlango kwa nguvu ndiyo sauti ya mtoto ikasikika ikilia mama ananichoma moto na mkubwa akaendelea kusema mama dada anamchoma moto mtoto,” alisema.
MAJIRANI WAKIMBILIA KWA MJUMBE
Mama huyo alisema, baada ya kumkosa kwa njia ya simu majirani walikimbilia kwa mjumbe ambapo hawakumkuta wakaamua kurejea pale nyumbani.
BOSI AFIKA
Bi mkubwa huyo aliweka bayana kuwa wakati majirani wanarejea pale nyumbani, bahati nzuri na yeye akawa amefika. “Nilipofika nikiwa sina hili wala lile lililotokea nyumbani muda wa saa kumi na moja hivi nikagonga mlango ukawa haufunguliwi nilipoita Maua akaitika na kusema mama umerudi akafungua mlango.
“Nikawauliuzia watoto kwani sikuwaona akaniambia mmoja amelala na mwingine alikuwa amekwenda tuisheni kwani kulikuwa kumepoa lakini akajistukia na kuniambia huyu mtoto mdogo anaumwa hawezi hata kutembea alianguka alipokwenda kwa jirani. “Kiukweli nilichanganyikiwa nikamchukua na kumvua nguo kumuangalia amepatwa na nini kwani nilishakuwa na mawazo mengine. “Nilikuta mtoto ana majeraha ameumia hawezi hata kutembea.
Nilimbana dada wa kazi ili aseme ukweli lakini alikataa katakata na kusema kuwa hajamfanya lolote, wakati namuuliza majirani wakaja wakanikuta na kuanza kumpiga Maua tukambemba mpaka kwa ili aseme kilichomkuta mtoto.
ASEMA UKWELI
“Alipofika kwa mtendaji msichana huyo alikataa katakata lakini alipobanwa na walinzi shirikishi alikubali na kusema amempiga na mwiko na huwa anawapiga kila siku na kuwazuia wasiseme kila wanapokataa kula chakula.
MTOTO MKUBWA ATOA USHUHUDA
“Mtoto mkubwa alipotakiwa kutoa ushuhuda wa kilichotokea akasema dada amekuwa akiwapiga kila siku na kusimulia mkasa mzima wa siku hiyo ambapo dada aliwapiga na kumchoma moto mtoto mdomoni pamoja na mkononi lakini mwisho pia alimpiga mtoto na mwiko wa kupikia kwenye mashughuli (mwiko mkubwa anaoutumia mama yao) na mwiko huo umevunjika,” alisema.
Baada ya ushuhuda wa mtoto na dada wa kazi kukiri kisha kuomba msamaha, mama Karan na majirani walimpeleka Maua Kituo cha polisi Mbezi kwa Yusufu ambapo alifunguliwa kesi kwa namba ya faili iliyosomeka RB: KMR/RB/10570/2017 KUJERUHI ili sheria ichukue mkondo wake.
MTOTO APELEKWA HOSPITALI
Kutokana na majeraha mbalimbali aliyoyapata mwilini mtoto huyo, mama yake alilazimika kuchukua kibali cha polisi na kumkimbiza Hospitali ya Palestina kwa ajili ya matibabu. Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, ACP Murilo Jumanne ili kuzungumzia tukio hilo, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa ila tunaamini Jeshi la Polisi lililo chini ya IGP Simon Sirro litatenda haki ili kama binti huyo amefanya ukatili huo, sheria stahili zichukuliwe ili iwe fundisho kwa wengine.
NENO LA MHARIRI
Kutokana na matukio ya aina hii kuanza kushamiri, ni vyema wazazi wakawa makini na wasichana wa kazi wanaowaajiri kwa kufuatilia mienendo ya watoto wao na mabinti hao kudhibiti matukio haya.
Post a Comment