Header Ads

Auawa kisha kutupwa msituni

                             

MKAZI wa kijiji cha Kateka wilayani Kalambo mkoani Rukwa, Gerad Konza (70), aliuawa kwa kucharangwa mapanga na watu wasiofahamika kisha mwili wake kutupwa shambani.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Tarafa ya Matei, Andrew Ngindo alisema maiti ya Konza iligunduliwa na wachungaji waliokuwa wakilisha mifugo yao kwenye mashamba yaliyopo eneo la Katete.

Alisema wafugaji hao walipokuta mwili huo ukiwa na majeraha walitoa taarifa kwenye kijiji ambako kulipigwa la mgambo na watu kukusanyika.

Alisema baadaye kijiji kilitoa taarifa polisi ambao walifika katika eneo hilo wakiwa na daktari ambaye baada ya uchunguzi alithibitisha kuwa marehemu alikufa kutokana na kupoteza damu nyingi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha kutokea mauaji hayo na kusema kuwa upelelezi wa kuwabaini wauaji ili wachukuliwe hatua za kisheria unaendelea.

Alisema hakuna watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba baada ya uchunguzi wa kitabibu ilibainika kwamba marehemu alipoteza maisha baada ya kutokwa damu nyingi kufuatia majeraha ya mapanga aliyocharangwa.

Kamanda Kyando aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi akidai kuwa kuendesha vitendo vya kuwaua watu ni kosa kisheria na kuwa kwa sasa jeshi linaendelea na msako kwa wahusika wa tukio hilo.

No comments