Takwimu za mchanga wa madini zatiliwa shaka...
Wadau wa masuala ya madini nchini wameshauri kubadilishwa kwa mfumo wa uchimbaji madini ili kuondokana na mfumo wa sasa ambao una mbinu nyingi za kukwepa kodi.
Ushauri huo umetokana na maazimio yaliyotolewa jana katika kongamano la rasilimali za madini lililoitishwa na chama cha ACT-Wazalendo na kuwashirikisha wadau wa masuala ya madini akiwamo Dk Rugemeleza Nshala, Dennis Mwendwa na Nico Kajungu.
Maazimio hayo yameshauri serikali kubadilisha mfumo wa uchimbaji madini kwa kuhamia kwenye mfumo wa kugawana mapato.
Pia wadau hao wamekosoa takwimu zilizotolewa na kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma, kuhusu kiwango cha madini kwenye makinikia.
“Takwimu zilizotolewa na Kamati ya Profesa Mruma, licha ya mchango wake katika kuibua mjadala, zina walakini. Takwimu hizi, zikukubaliwa kama zilivyo, zinaifanya Tanzania kuwa mzalishaji namba moja wa dhahabu Afrika,” yamesema maazimio hayo
Wadau hao walitoa azimio la kuwepo kwa timu huru ya kupitia takwimu zilizotolewa na Kamati ya Profesa Mruma ili kuthibitisha uhalali wake.
Maazimio mengine ni kufanya mabadiliko ya sheria ya madini na katiba ili kuyafanya madini na maliasili nyinginezo kuwa mali ya wananchi milele.
Mengine ni watu wote walioshiriki katika kuingia mikataba ya madini na kufanya maamuzi yanayolitia hasara taifa wawajibishwe na kuchukuliwa hatua bila kujali vyeo vyao au lini makosa hayo yalifanyika.
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliongoza kongamano hilo.
Post a Comment