Header Ads

Kesi ya Mmiliki wa Lucky Vincent na makamu wake yabamba



Arusha. Mmiliki wa Shule ya Lucky Vincent, Innocent Mosha na Makamu mkuu wa shule hiyo, Logino Vicent leo wamepandishwa tena kizimbani kujibu mashtaka matano yanayohusu ajali ya basi iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja mwezi uliopita.

Kesi hiyo, imesomwa leo Alhamisi mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa Arusha, Desderi Kamugisha, ambapo Wakili wa Serikali Rose Sulle amesema watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa matano tofauti.

Amesema mmiliki wa shule hiyo, anakabiliwa na makosa matano, ambayo ni kutokuwa na leseni ya usafirishaji wa gari lake lililopata ajali, kosa la pili ni kushindwa kuwa na leseni ya barabarani,
makosa mengine ni mmiliki wa shule hiyo kushindwa kuingia mkataba na dereva wake Dismas Joseph aliyepoteza maisha kwenye ajali hiyo, pia kuzidisha abiria 13 katika gari lililopata ajali.

Sulle amesema, makamu mkuu wa chuo, Vicent anakabiliwa na shtaka moja la kuidhinisha kusafirishwa kwa abiria wengi kwenye basi hilo.

Hata hivyo, Sulle aliomba kesi hiyo kupangwa tarehe nyingine kutokana na kutokamilika kwa upelelezi.

Hakimu Kamugisha alikubaliana na ombi la mwendesha mashtaka huyo na kutaka washtakiwa hao warudi tena mahakamani Julai 5, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Ajali ya wanafunzi wa shule hiyo, ilitokea Mei 6, katika eneo la Rhotia wilayani Karatu, mkoani Arusha.

No comments