Header Ads

HansPope afunguka asema Ndikumana ndiye anayeitaka Simba



MWENYEKITI WA KAMATI YA USAJILI YA KLABU YA SIMBA, ZACHARIA HANSPOPE.

MWENYEKITI wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba, Zacharia HansPope, amesema viongozi wa timu hiyo hawajafanya mazungumzo na beki wa Mbao FC raia wa Burundi, Yusuph Ndikumana ila mchezaji alimpigia simu kuomba kuonana naye.

Hivi karibuni kumeibuka taarifa za uongozi wa Simba kufanya mazungumzo na mchezaji huyo kitu ambacho HansPope amekikana.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, HansPope, alisema kuwa meneja wa mchezaji huyo amekuwa akilalamika kuwa viongozi wa Simba wanamsumbua nyota huyo wakitaka kumsajili.

“Hakuna kiongozi aliyefanya mazungumzo na Ndikumana, ila nikiwa Burundi hivi karibuni kwa shughuli zangu binafsi, Ndikumana alinipigia simu akitaka tuonane, lakini kwa sababu nilisikia malalamiko ya meneja wake, nilimwambia kama ni suala la usajili siwezi kuonana naye, kifupi hakuna kiongozi aliyemtafuta Ndikumana kutaka kumsajili, ila yeye ndiye anayeitaka Simba,” alisema HansPope.

Alisema malalamiko ya meneja wa mchezaji huyo kuwa Simba wanamzunguka na kufanya naye mazungumzo si ya kweli.

“Kwa mchezaji yeyote tutakayemtaka tutafuata utaratibu unaokubalika,” aliongeza kusema Hanspope.

Ndikumana ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji wanaotajwa zaidi kutaka kujiunga na timu moja wapo kati ya Simba na Yanga kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kwenye kikosi cha Mbao FC. .

No comments